Habari ya Asubuhi na karibu kwenye matangazo yetu Mubashara hii leo….
Kamati iliyokuwa inachunguza ajali ya ndege Jumatano wiki hii nchini Urusi, imethibitisha kuwa Yevgeny Prigozhin, aliyekuwa kiongozi wa mamluki wa Wagner, alikuwa miongoni mwa watu walioangamia.
Watalaam wa Kamati hiyo wamesema, uchunguzi wa mabaki baada ya ajali hiyo, umebaini kuwa Prigozhin, alikuwa miongoni mwa abiria waliopotea maisha baada ya kuanguka kwa ndege hiyo.
Msemaji wa Kamati hiyo Svetlana Petrenko amesema, orodha ya majina ya watu 10 waliokuwa kwenye ndege hiyo kabla haijaanguka, wametambuliwa wakiongozwa na Prigozhin pamoja na msaidizi wake Dmitry Utkin.
Ndege hiyo alianguka na kumuua, Prigozhin miezi miwili baada ya kujaribu kulipindua jeshi la Urusi, baada ya kuhitilafiana kuhusu vita nchini Ukraine. Licha ya ripot hii, haijafahamika kilichosababisha ajali hiyo.
Wiki hii rais Vladimir Putin, akimwomboleza kiongozi huyo wa zamani wa Wagner, alimwelezea kama mfanyabiashara mahiri ambaye alifanya makosa makubwa kwenye maisha yake.
Kumekuwa na uvumi kuwa huenda Putin alihusika na ajali, kufuatia kitendo cha Prigozhin kujaribu kutikisa uongozi wake, lakini madai hayo hayajathibitishwa.