Mwanamume mmoja katika kaunti ya Kirinyaga alijikuta katika hali mbaya baada ya kukatwa mkono kwa kushukiwa kuiba mirungi.
Kwa mijibu wa vyanzo vya habari, kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 sasa anapigania maisha yake katika hospitali moja kwenye kaunti hiyo, hii ni baada ya kuvamiwa na umma uliomfumania akiiba zao la Miraa ambalo ni kitega uchumi kwa wakaazi wengi wa kaunti jirani ya Meru.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Mwea-mashariki James Mutua alimtaja mshukiwa kuwa Stanley Maina kutoka kijiji cha Ngucui huko Murinduko,
Kulingana na mkuu wa polisi, umati huo ulivamia nyumba ya kukodi ya Maina jana usiku na kumvuta nje kwa tuhuma kwamba alikuwa ameiba miraa katika kijiji cha Mugumo-ini.
Wakazi hao pia walimshtumu mshukiwa huyo kwa kuwa mwizi mdogo kijijini akiiba kuku na kila kitu alichokutana nacho, ripoti hiyo ilisema Zaidi.
Wakaazi baadaye walimiminika katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kimbimbi ambapo mshukiwa alikuwa amekimbizwa kwa matibabu.
Kamanda wa polisi James Mutua alisema maafisa wake wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Katika eneo hilo lenye wingi wa mirungi, ni kawaida kwa mtuhumiwa wa wizi wa mirungi kukabidhiwa adhabu ya kukatwa kiungo cha mwili kama njia moja ya kutoa funzo kwa wezi wengine, suala ambalo hata hivyo limeonywa vikali na kamanda huyo wa polisi akiwatahadharisha wananchi dhidi ya kuchukua sheria mikononi.