Idara ya usalama ya Urusi FSB imemfungulia mashtaka mfanyakazi wa zamani wa ubalozi mdogo wa Marekani kwa kukusanya taarifa kuhusu vita vya Ukraine huko Washington, shirika la habari la serikali TASS lilisema.
Mshukiwa huyo, Robert Shonov, anadaiwa kupitisha taarifa kwa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani mjini Moscow kuhusu jinsi kampeni ya kuwaandikisha watu jeshini Urusi ilivyoathiri hali ya kutoridhika kisiasa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2024, TASS ilinukuu FSB ikisema.
FSB ilisema inapanga kuwahoji wafanyikazi wa ubalozi ambao walikuwa wakiwasiliana na Shonov.
Mwezi Mei, ubalozi ulisema “madai dhidi ya Bw. Shonov hayana mashiko kabisa”, na “jukumu lake pekee wakati wa kukamatwa kwake lilikuwa kukusanya muhtasari wa vyombo vya habari kutoka kwa vyanzo vya habari vya Urusi vinavyopatikana hadharani”.
FSB ilichapisha video ya kukamatwa kwa Shonov na ushuhuda ambapo aliwataja wafanyakazi wa Ubalozi wa Marekani Jeff Sillin na David Bernstein kama watu ambao walitafuta huduma yake mnamo Septemba 2022.
“Ilinibidi kukusanya habari hasi, kutafuta kutoridhika na kuionyesha katika ripoti zangu,” Shonov alisema.
FSB ya Urusi ilisema imetuma maombi kwa Ubalozi wa Marekani huko Moscow kuwahoji Sillin na Bernstein.
Shonov alikuwa amefanya kazi kwenye ubalozi mdogo wa Marekani huko Vladivostok kwa zaidi ya miaka 25 hadi 2021, wakati Moscow iliweka vizuizi kwa wafanyikazi wa ndani wanaofanya kazi kwa misheni za kigeni.