Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji Askari wa kampuni ya ulinzi PASCO LTD 11, Maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wawili na askari Polisi 6 Kushikiliwa kwa watu hao kunatokana na tuhuma za kujeruhiwa kwa watu wawili ambao baadae walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali ya Mloganzila. Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kanda Maalum Dar es salaam, Jumanne Muliro Jumanne.
“Tarehe 28 Agosti, 2023 Majira ya saa 8 usiku eneo la Kiluvya Ubungo, maafisa kutoka katika taasisi hizo wanadai wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, lilitokea kundi la watu wanaokadiriwa kuwa 30 wakiwa na Pikipiki zilizokuwa zimebeba magunia ya mkaa ambayo ni mazao ya misitu na walipofika eneo la ukaguzi na kuamriwa wasimame, walikaidi na kuanza kufanya fujo kubwa kwa kuwarushia mawe Maofisa wa maliasili na wenzao wakishinikiza pikipiki zilizo kuwa na mkaa kinyume na sheria ziachiwe, Mafisa wa timu hiyo waliokuwa na silaha walianza kufyatua risasi kwa lengo la kuwatawanya na kujilinda Hata hivyo ilibainika watu wawili walijeruhiwa katika purukushani hizo na walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali ya Mloganzila”