Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bw. Filippo Grandi jana alitoa wito wa dola bilioni moja za kimarekani kusaidia waliorejea na wakimbizi waliokimbia mgogoro wa Sudan na kuelekea nchi jirani.
Bw. Grandi alisema katika mji mkuu wa Sudan Kusini wa Juba kwamba, kutokana na ongezeko kubwa la watu kutoka Sudan, UNHCR imemaliza rasilimali zote ilizokusanya hapo awali na sasa inahitaji fedha zaidi.
Alibainisha kuwa kati ya fedha hizo, Sudan Kusini itapokea dola milioni 356 za kimarekani wakati zilizosalia zinaweza kwenda nchi nyingine kama vile Chad na Misri, ambazo pia zinapokea wakimbizi kutoka Sudan.
Sudan Kusini, kulingana na Grandi, hadi sasa imepokea takriban watu 400,000, wengi wao wakiwa ni raia wa Sudan Kusini waliorejea kutoka nchi jirani ya Sudan.
Kwa upande wake, Waziri wa Masuala ya Kibinadamu na Usimamizi wa Majanga wa Sudan Kusini, Albino Akol Atak alisema baraza la mawaziri limetoa zaidi ya dola milioni 5 kusaidia operesheni za kibinadamu kwa wakimbizi na wanaorejea kutoka Sudan.
“Fedha ambazo ziliidhinishwa na baraza la mawaziri zimeshughulikia shughuli za kibinadamu, haswa kuwapokea na kuwasafirisha wakimbizi na wanaorejea kutoka sehemu za kuingilia Joda huko Upper Nile na katika eneo lingine katika majimbo ya Unity, Warrap, Kaskazini na Magharibi ya Bahr el Ghazal”, aliambia. waandishi wa habari siku ya Jumanne.
Zaidi ya watu milioni 4.5 wameripotiwa kuyahama makazi yao ndani na nje ya Sudan kutokana na mzozo uliozuka Aprili 15 kati ya jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (SAF).