Mgogoro wa kisiasa unaoendelea, bila suluhu ya wazi inayoonekana, unazua sintofahamu na wasiwasi huku Niger ikiendelea kukumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi yasiyo ya kiserikali, hasa karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso, ilisema UNHCR.
Ghasia za hivi majuzi zimesababisha ongezeko la watu 20,000 wapya waliokimbia makazi yao katika mwezi uliopita kulingana na Bw. Gignac, ambaye alibainisha kuwa ongezeko la matukio ya usalama katika wiki chache zilizopita kumeongeza hatari za ulinzi kwa wakimbizi, wanaotafuta hifadhi na wenyeji wao.
Kwa mfano, mwezi Julai UNHCR ilifuatilia matukio 255 ya ulinzi ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa majumbani.
Tangu kuondolewa madarakani kwa rais Mohamed Bazoum, aliyechaguliwa kidemokrasia hapo Julai 26, kumekuwa na hali ya taharuki, amesema mwakilishi wa UNHCR nchini Niger Emmanuel Gignac.
Ameongeza kusema kwamba ni vigumu kubashiri hali itakavyokuwa, na kwamba UNHCR na UN wameweka mikakati ya kukabiliana na dharura inayoweza kutokea.
Bw. Gignac alisisitiza kuwa akiba ya UNHCR ya vitu muhimu, inayohudumia takriban familia 5,000, inatarajiwa kudumu kwa miezi mitatu hadi mitano.
Aidha ameeleza kusikitishwa kwake na upatikanaji wa dawa na huduma za afya huku akihimiza kuendelea kwa huduma za afya ambazo zimezoeleka kutolewa na serikali licha ya vikwazo hivyo.