Rais wa Gabon Ali Bongo yuko chini ya kizuizi cha nyumbani na mmoja wa wanawe amekamatwa kwa “uhaini”, maafisa wa kijeshi walisema Jumatano, saa chache baada ya kutangaza kuwa wamepindua serikali.
“Rais Ali Bongo yuko chini ya kizuizi cha nyumbani, amezungukwa na familia yake na madaktari,” walisema katika taarifa iliyosomwa kwenye runinga ya serikali.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa watu wengine serikalini wamekamatwa kwa tuhuma mbalimbali.
China imetoa wito kwa pande zote nchini Gabon kutoa usalama kwa rais Ali Bongo, wito unaokuja baada ya kundi la wanajeshi kudai kumaliza utawala wa sasa kwenye taifa hilo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin ameeleza kuwa nchi yake pia inafuatilia kwa ukaribu hali inayoendelea nchini Gabon.
Beijing inapendekeza kufanyika kwa mazungumzo ya pande zote nchini humo kwa manufaa ya raia na kurejeshwa kwa hali ya kawaida haraka iwezekanavyo.
Bongo aliongoza taifa hilo la Afrika kama rais kwa kipindi cha muda wa miaka 14 na alikuwa ametangazwa tena mshindi wa uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Kiongozi huyo alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2009 baada ya kifo cha baba yake, Omar Bongo Ondimba, amabye alikuwa ameongoza taifa hilo kwa kipindi cha miaka 41.