Baadhi ya akina mama wa wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wameanza mgomo wa kususia kula wakipinga hali mbaya ya magereza na kuwaunga mkono watoto wao.
Tangu tarehe 7 Agosti, zaidi ya wafungwa 800 wa kisiasa katika Gereza Kuu la Jo nchini Bahrain walianza mgomo wa kususia kula kwa muda usiojulikana chini ya kauli mbiu ya “Tuna Haki” baada ya viongozi wa nchi hiyo kupuuza madai yao na kuendeleza mateso na manyanyaso dhidi yao.
Akina mama kadhaa wa wafungwa wa kisiasa wameanza mgomo wa kususia kula wakilalamikia hali mbaya ya magereza na kuwaunga mkono watoto wao ambao wamegoma kula kwa muda wa siku 23 sasa.
Kuhusiana na suala hilo, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Bahrain Ibtisam Al-Saigh amesema: wito wa kutangaza mshikamano na wafungwa wa kisiasa unazidi kuenea; na mgomo wa kususia kula si wenzo tena kwa wanaonyimwa haki zao, bali ni wenzo wa kuuamsha ubinadamu.
Wanaharakati wa kiraia na kisiasa wa Bahrain katika miji ya Berlin Ujerumani, London Uingereza na Melbourne Australia, nao pia wameanza mgomo wa kususia kula kwa sura ya kimaigizo ili kuonyesha mshikamano na wafungwa wa kisiasa wa Bahrain.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgomo huo unaoendeshwa kwa kauli mbiu ya “Tuna Haki”, ambao ulizinduliwa na mamia ya wafungwa wa kisiasa wakilalamikia mazingira yasiyoridhisha, unaingia wiki ya nne kutokana na viongozi wa Bahrain kukataa kutekeleza matakwa ya wafungwa hao.