Ikulu ya White House imeionya Korea Kaskazini dhidi ya kuiuzia Urusi silaha kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine huku mvutano kati ya Pyongyang na Washington ukiendelea kushika kasi.
Msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby alisema Jumatano kwamba Marekani ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa makubaliano ya silaha kati ya Urusi na Korea Kaskazini.
“Tunaitaka DPRK kusitisha mazungumzo yake ya silaha na Urusi na kutii ahadi za umma ambazo Pyongyang imetoa kutotoa au kuiuzia Urusi silaha,” Kirby alisema, akimaanisha Korea Kaskazini kwa jina rasmi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea. .
Kirby aliongeza kuwa Marekani inaamini kuwa Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu alijaribu kuishawishi Pyongyang kuiuzia Moscow risasi za kivita alipotembelea Korea Kaskazini na kukutana na kiongozi wake Kim Jong Un mwezi Julai.
Msemaji wa Ikulu ya White House alikataa kueleza kwa undani jinsi maafisa wa Marekani walivyokusanya taarifa hizo za kijasusi.
Marekani imekuwa ikiwaonya washindani wake na wapinzani – ikiwa ni pamoja na China – dhidi ya kuisaidia Urusi katika mashambulizi yake ya kijeshi nchini Ukraine.