Kundi la wadukuzi linaloitwa Anonymous Sudan lilidukua mtandao wa X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter, katika zaidi ya nchi kumi na mbili Jumanne asubuhi katika jaribio la kumshinikiza Elon Musk kuanzisha huduma yake ya Starlink nchini mwao.
X ilikuwa haipatikani kwa zaidi ya saa mbili, na maelfu ya watumiaji walioathirika.
“Fanya ujumbe wetu umfikie Elon Musk: ‘Fungua Starlink nchini Sudan’,” wadukuzi hao walichapisha kwenye Telegram.
X ndio mtandao mwathirika wa hivi punde zaidi wa genge lililoshambulia ili “kunufaisha Sudan na Uislamu”.
Kwa wiki kadhaa za mazungumzo ya faragha na kikundi kwenye programu ya mazungumzo ya Telegram, BBC ilizungumza na wadukuzi kuhusu mbinu na nia zao.
Mwanachama wa kundi la wadukuzi – Hofa – alisema shambulio lililoitwa DDoS (Distributed Denial of Service) lililenga kuongeza ufahamu kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ambavyo “vinafanya mtandao kuwa mbaya sana na unashuka mara kwa mara kwa ajili yetu”.
X haijakiri hadharani kuhusu hitilafu na usumbufu uliosababishwa, na Bw Musk hajajibu maswali ya kuzindua huduma yake ya mtandao wa satelaiti nchini Sudan.