Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika linakutana Alhamisi kuchunguza hali nchini Gabon, siku moja baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua rais Ali Bongo Ondimba, AU imetangaza katika taarifa yake.
“Kwa wakati huu – Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika linakutana kuchunguza hali nchini Gabon,” AU imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotangazwa kwenye X (zamani ikiitwa Twitter).
Mkutano huo unaongozwa na Kamishna wa Masuala ya Kisiasa wa Umoja wa Afrika, Bankole Adeoye wa Nigeria, na mwenyekiti wa sasa wa baraza hilo, Willy Nyamitwe (kutoka Burundi), inaongeza taarifa, bila maelezo zaidi.
Siku ya Jumatano, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, “alilaani vikali” kile alichokitaja kama “jaribio la mapinduzi ya kijeshi” nchini Gabon, nchi ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa mafuta, ambayo imeongozwa kwa zaidi ya miaka 55 na Familia ya Bongo.
Siku ya Jumatano viongozi wa mapinduzi walitangaza kwamba “wamezima utawala uliokuwa ukiongoza” nchini Gabon na wamemweka rais Ali Bongo Ondimba, madarakani kwa miaka 14, chini ya kizuizi cha nyumbani, mara tu baada ya kutangazwa rasmi ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi.
Moussa Faki Mahamat pia alitoa wito kwa jeshi la Gabon na vikosi vya usalama “kuhakikisha uadilifu wa kimwili” wa Ali Bongo Ondimba.