Robo ya wananchi wote wa Somalia wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na ukame na migogoro.
Hayo yamesemwa na shirika la kibinadamu la Islamic Relief katika ripoti yake mpya na kueleza kuwa, watu milioni 4.3 wamehama makazi yao katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kutokana na ukame na utovu wa usalama.
Shirika hilo lenye makao yake nchini Uingereza limebainisha kuwa, takwimu hizo mpya zinaashiria kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo cha watu kuhama makazi yao kutokana na ukame na migogoro ya kivita.
Farhan Abdirizak Adan, Afisa wa Miradi wa Islamic Relief amesema ukame si tu umeua watu na mifugo na kuharibu mimea nchini Somalia, lakini pia umepelekea kupanda kwa bei za chakula.
Ameongeza kuwa, hali katika mji wa Baidoa unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku, kutokana na mji huo ulioko magharibi mwa mji mkuu Mogadishu kupokea idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 40 ya wananchi wa Somalia wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.
Haya yanajiri huku Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) likitahadharisha kuwa, mabadiliko ya tabianchi ya El Nino yanayotazamiwa kushuhudiwa kuanzia mwezi ujao wa Oktoba, yataathiri watu milioni 1.2 na ekari milioni 3.7 za ardhi ya kilimo nchini humo.