Mkutano wa kwanza wa kilele kuhusu tabianchi barani Afrika unafunguliwa Nairobi, Kenya Jumatatu hii, Septemba 4. Kwa siku tatu, viongozi kutoka Afrika na kwingineko watakutana ili kujadiliana na wahusika kutoka mashirika ya kiraia pamoja na makampuni ya umma na ya kibinafsi, na mashirika ya kimataifa. Madhumuni yaliyotajwa: kuafikiana kwenye mtazamo mmoja kwa bara la Afrika, kwa kuweza kuuwasilisha kwa mkutano mwingine uliopangwa kufanyika mwezi Desemba huo Dubai.
Takriban viongozi ishirini wa nchi na serikali wa Afrika na karibu wajumbe 20,000 kutoka duniani kote wanakutana Nairobi.
Rais wa Kenya William Ruto, ambaye nchi yake ni mwenyeji wa hafla hiyo, ndiye anayeongoza katika pambano hili na anataka mkutano huu ulete mabadiliko kwa jinsi bara la Afrika linavyojipanga katika masuala ya mazingira.
Iwapo hili litatimia, itakuwa ni dhamira dhabiti barani Afrika, chini ya miezi mitatu kabla ya COP28, ambayo inaanza mwishoni mwa Novemba huko Dubai.
Nchi za bara la Afrika ni miongoni mwa nchi zilizo hatarini zaidi na mabadiliko ya tabianchi: ukame, mafuriko, vimbunga… majanga ya asili yanaongezeka barani humo.
Hata hivyo, kwa kuongeza, kuna ukosefu wa njia za kujibu, hasa kwa vile nchi kadhaa zinakabiliwa na uzito wa madeni yao.
Hitaji la usanifu mpya wa kifedha kwa ajili ya hali ya hewa kwa hivyo linapaswa kuwa kiini cha majadiliano, karibu na urekebishaji wa madeni, kwa mfano, au uanzishaji wa ushuru kwenye mafuta ya kisukuku na tasnia zinazochafua mazingira, kama vile usafiri wa anga na baharini.
Mkutano huo unanuia kuangazia uwezo wa bara hilo katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.