Baada ya kuwepo kwa kilio cha Wakulima wa zao la Tumbaku katika Wilaya ya Kahama Halmashauri ya Ushetu kutolipwa fedha zao na Makampuni yanayohusika na ununuzi wa zao hilo, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Peter Cherehani ameiomba serikali kuingilia kati suala hilo na kuwasaidia wakulima hao kupata fedha zao.
Mhe. Cherehani amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliowahusisha pia na wakulima wa zao hilo na kuongeza kuwa ni zaidi ya miezi minne hivi sasa wakulima hao bado hawajalipwa fedha zao licha ya kuuza mazao yao kwa makampuni wanunuzi huku wakiendelea kukumbwa na ongezeko la riba kutoka kwenye mabenki mbalimbali.
“Wakulima hawa walishafanya kazi yao lakini mpaka leo makampuni mawili hawajawalipa fedha zao kiasi cha kupelekea kukumbwa na ongezeko la riba hivyo niiombe Serikali, riba hiyo ilipwe na makampuni hayo sambamba na fedha za wakulima hawa ambao wameuza zaidi ya Dola Milioni 18”, amesema Mhe. Cherehani.