Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Sputnik siku ya Jumatatu, magaidi 150 wa kundi la Al-Shabaab waliuawa nchini Somalia katika operesheni ya kijeshi katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hii, siku mbili zilizopita, magaidi 20 wa kundi hili waliuawa katika operesheni ya pamoja ya anga ya jeshi la Somalia na washirika wa kimataifa.
Vyanzo vya habari pia viliripoti usiku wa Jumamosi iliyopita kwamba wanachama 13 wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab waliuawa katika operesheni za jeshi la Somalia la nchi hiyo.
Inasemekana magaidi hao waliuawa wakati wa operesheni za anga na ardhini za jeshi la Somalia katika jimbo la Lower Juba kusini mwa nchi.
Mwishoni mwa mwezi wa Julai mwaka huu, jeshi la Somalia lilitangaza kuuawa magaidi 100 wa Al-Shabaab wakati wa operesheni ya kijeshi katika eneo la Fima kati ya majimbo mawili ya Shabelle ya Kati na Gholghdod katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Katika mwezi huo huo wa Julai, magaidi wengine 60 wa al-Shabaab waliuawa pia katika operesheni iliyotekelezwa na jeshi la Somalia katika eneo la Bay, kusini mwa nchi.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo lina mielekeo ya itikadi kali na mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, limekuwa likijaribu kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007 na limeshafanya operesheni nyingi za kigaidi na kuua idadi kubwa ya wanajeshi na raia wa nchi hiyo.