Waziri Mkuu aliyeteuliwa na jeshi la Niger siku ya Jumatatu alisema aliona matumaini ya kupatikana kwa makubaliano na jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, ambayo imetishia kutumia nguvu kurejesha utawala wa kiraia baada ya mapinduzi mwezi Julai.
“Hatujasitisha mawasiliano na ECOWAS, tunaendelea na mawasiliano. Tuna matumaini mazuri ya kufikia makubaliano katika siku zijazo,” Waziri Mkuu Ali Mahaman Lamine Zeine aliuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Niamey.
ECOWAS Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi imeweka vikwazo vikali dhidi ya Niger baada ya wanajeshi waasi Julai 26 kumpindua Mohamed Bazoum, rais wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia.
Pia imeonya mara kadhaa ya kuingilia kijeshi kuirejesha Bazoum, lakini tu ikiwa majaribio ya amani ya kutatua mgogoro huo yatashindwa.
“Tunajipanga kushambuliwa wakati wowote. Kila maandalizi yamechukuliwa. Itakuwa ni vita isiyo ya haki. Tumedhamiria kujilinda ikiwa kutakuwa na shambulio,” Zeine aliwaambia waandishi wa habari.
Swali kuu katika mgogoro huo ni ratiba ya kurudi kwa utawala wa kiraia.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS Alhamisi iliyopita alipendekeza kipindi cha miezi tisa kama vile nchi yake ilivyopitia mwishoni mwa miaka ya 1990.
“Rais haoni sababu kwa nini hali kama hiyo haiwezi kuigwa nchini Niger, ikiwa mamlaka ya kijeshi ya Niger ni waaminifu,” ofisi ya rais wa Nigeria ilisema katika taarifa.
Algeria, jirani mwenye ushawishi mkubwa wa kaskazini mwa Niger, imependekeza kipindi cha mpito cha miezi sita.
Watawala wa kijeshi hadi sasa hawajajibu mapendekezo hayo, baada ya kuzungumza juu ya kipindi cha miaka mitatu ya kurudi nyuma.
ECOWAS imechukua msimamo mkali kuhusu Niger kufuatia msururu wa mapinduzi katika eneo lake tangu 2020.