Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 1.8 watakuwa wameikimbia Sudan kutokana na mapigano ya silaha ya kuwania madaraka nchini humo, ambayo yamekuwa yakiendelea tangu Aprili 15 kati ya vikosi vya jeshi na vya Msaada wa Haraka RSF.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilisema hayo jana Jumatatu na kueleza kuwa, idadi ya watu wanaotoroka vita na mapigano nchini Sudan imeongezeka maradufu, kinyume na makadirio ya taasisi hiyo ya wakimbizi ya mwezi Mei, muda mfupi baada ya kuanza vita hivyo.
UNHCR imesema zaidi ya watu milioni moja tayari wameikimbia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kuelekea katika nchi za Chad, Misri, Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kwa mujibu takwimu za Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya UN, mapigano hayo yamelazimisha watu zaidi ya 170,000 kukimbilia nchi jirani ya Sudan Kusini.
UN inasema idadi ya wakimbizi wanaowasili Sudan Kusini kutokea Sudan inatazamiwa kuendelea kuongezeka kutokana na kuwa, mgogoro wa vita vya ndani huko Sudan bado haujapatiwa ufumbuzi.