Brazili kwa mara nyingine tena imekumbwa na tukio la hali mbaya ya hewa, baada ya kimbunga kusababisha vifo vya watu 21 kusini mwa nchi hiyo, ambapo mvua kubwa imesababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko ya kutisha katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
“Kwa bahati mbaya, nilipata taarifa kwamba miili 15 ilipatikana katika manispaa ya Muçum, ambayo inafanya idadi ya waliofariki kufikia 21,” Gavana wa jimbo la Rio Grande do Sul, Eduardo Leite, alisema siku ya Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari.
Kimbunga hiki, ambacho kilianza kuathiri jimbo hili linalopatikana kwenye mpaka na Uruguay na Argentina siku ya Jumatatu, kilisababisha “majanga tupu huko Rio Grande do Sul”, aliongeza.
Mnamo mwezi Juni, kimbunga kingine kilisababisha vifo vya watu 16 katika jimbo hilo.
Gavana alibainisha kuwa maafisa kadhaa wa kikosi cha Zima moto walihamasishwa na kwamba “watu mia kadhaa” wameokolewa.
Helikopta zilitumika kuwahamisha wakazi, huku baadhi ya barabara zikiwa hazitumiki kabisa kutokana na mafuriko.
Zaidi ya watu 50,000 kutoka karibu miji sitini waliathiriwa na zaidi ya 3,700 kati yao walilazimika kutoroka makaazi yao, kulingana na ripoti ya hivi punde kutoka serikali za mitaa.