Magaidi 53 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika mapigano ya karibuni kabisa yaliyotokea baina yao na jeshi la Burkin Faso.
Katika taarifa yake ya jana, jeshi la Burkina Faso limesema kuwa mapigano makali yalitokea Jumatatu kati yao na magaidi kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makumi ya magaidi wameangamizwa katika mapigano yaliyotokea kwenye eneo la Koumbri la jimbo la Yatenga, na kuongeza kuwa hadi jana Jumanne operesheni za kuwasafisha magaidi hao zilikuwa zinaendelea.
Tangu mwaka 2015, nchi ya Burkina Faso ya magharibi mwa Afrika haina usalama. Mashambulizi ya kigaidi yanatokea mara kwa mara na yameshasabasisha vifo vya watu wengi na kupelekea maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.
Shirika la Habari la Burkina lilisema kuwa, watu 18 wenye silaha walijeruhiwa kwenye shambulio hilo la kwanza na walikuwa chini ya ulinzi mkali wakipatiwa matibabu.
Vyombo vingine vya habari vya ndani ya Burkina Faso viliripoti kuwa, takriban watu wengine 20 waliuawa mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu katika eneo la Wakara la mkoa huo huo kwenye shambulio jingine la watu wenye silaha.
Duru moja ya serikali ilisema kuwa, makumi ya magaidi waliangamizwa na vikosi vya ulinzi na usalama vilivyojibu mashambulizi hayo.