Kivuko kikuu cha mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan kimefungwa baada ya vikosi vya usalama kutoka nchi zote mbili kurushiana risasi, maafisa walisema.
Wakaazi wa eneo hilo upande wa Pakistani waliripoti mlio wa risasi kwenye kivuko cha Torkham siku ya Jumatano na walisema watu waliokuwa karibu na eneo la mpaka lenye shughuli nyingi karibu na Khyber Pass walikuwa wamekimbia mara tu risasi zilipoanza.
Hakukuwa na ripoti za majeruhi, na haikujulikana mara moja kwa nini walinzi wa mpaka kutoka pande hizo mbili walirushiana risasi, alisema Nasrullah Khan, afisa wa Torkham, mji katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan.
Alisema maafisa wa serikali na jeshi la Pakistan walikuwa wakiwasiliana na wenzao wa Afghanistan ili kutuliza mvutano.
Sehemu ya mpaka wa Torkham ndio kituo kikuu cha kupitisha wasafiri na bidhaa kati ya Pakistani na Afghanistan isiyo na bandari.
Kivuko hicho kimefungwa mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kufungwa mnamo Februari ambayo ilishuhudia maelfu ya lori zilizobeba bidhaa zikiwa zimekwama kila upande wa mpaka kwa siku.