Kiongozi wa kijeshi Jenerali Brice Oligui Nguema, amemteua Raymond Ndong Sima, kuwa Waziri Mkuu mpya katika serikali ya mpito.
Sima amewahi kushika nafasi hiyo kati ya mwaka 2012 hadi 2014 , wakati wa uongozi wa Ali Bongo aliyeondolewa madarakani na jeshi.
Alikuwa mpinzani wa Bongo baada ya kundoka katika serikali yake, na wakati wa uchaguzi uliopita, alipinga kuchaguliwa kwake.
Wakati hayo yakijiri, msuluhishi wa mzozo wa Gabon, kutoka Jumuiya ya nchi za Afrika ya Kati, rais Faustin Archange Touadera, amekubaliana na kiongozi wa kijeshi Jenerali Brice Oligui Nguema kuhusu mchakato wa kurejesha nchi hiyo kwenye utawala wa kikatiba na kurejesha demokrasia.
Hatua hii imekuja baada ya Jumuiya hiyo ya ECCAS kumtuma mjumbe wake jijini Libreville ambaye alikutana na kuzungumza na Jenerali Oligui.
Baada ya wawili hao kukutana, haijawekwa wazi, kilichokubaliwa kati ya mjumbe huo ECCAS na kiongozi wa kijeshi wa Gabon, lakini imekubaliwa kuwa mchakato wa kurejesha demokrasia upangwe, suala ambalo lilikubaliwa na pande zote mbili.
Kufuatia hatua ya jeshi kuchukua madaraka, baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwezi uliopita, uliokuwa umempa ushindi rais Ali Bongo, Jumuiya ya ECCAS iliisimamisha Gabon uanachama.
Baada ya kuapishwa siku ya Jumatu, kuongoza serikali ya mpito, Jenerali Oligui aliahidi kuhakikisha kuwa uchaguzi huru na haki unafanyika nchini humo, lakini hakusema ni lini hili litafanyika.
Katika hatua nyingine, uongozi wa kijeshi umemuachilia huru aliyekuwa rais Ali Bongo baada ya kumuweka kwa kuzuizi cha nyumbani, na kusema yuko huru kuondoka nchini humo.