Mashirika ya misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yamelazimika kupunguza misaada huku kukiwa na mzozo wa kifedha na hali inayozidi kuwa mbaya ya kibinadamu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (Ocha) inasema.
Jumla ya watu milioni 7.76 wanakabiliwa na viwango vya janga la mahitaji, lakini upungufu wa rasilimali unamaanisha msaada wa dharura wa chakula sasa utapewa kipaumbele kwa watu milioni 3.2 ambao wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.
Hii ina maana wale tu walio kwenye ukingo wa njaa ndio watasaidiwa – na hata mgao wao unakatwa.
“Ukweli rahisi ni kwamba hakuna rasilimali za kutosha zinazopatikana kwa jumuiya ya kibinadamu ili kukidhi mahitaji nchini Sudan Kusini,” alisema Makena Walker, kaimu mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
“Viwango vilivyokithiri vya uhaba wa chakula na utapiamlo vinaathiri theluthi mbili ya wakazi wa nchi hiyo, na kuifanya kuwa moja ya dharura mbaya zaidi za uhaba wa chakula duniani.”
Umoja wa Mataifa ulikuwa umeomba $1.7bn (£1.3bn) lakini ni asilimia 46 tu ya ufadhili huo ndiyo umepokelewa.
Zaidi ya $300m pia zinahitajika kwa dharura kutoa msaada kwa watu wanaotoroka mpakani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.