Mwendesha mashtaka wa Uhispania amewasilisha malalamiko katika mahakama yake kuu dhidi ya rais wa shirikisho la soka aliyesimamishwa kazi Luis Rubiales kwa unyanyasaji wa kingono na kulazimishwa.
Rubiales alimbusu kiungo wa kati Jenni Hermoso kwenye midomo baada ya ushindi wa fainali ya Kombe la Dunia ya Wanawake ya Uhispania, ambayo anasema haikukubaliwa.
Hermoso aliwasilisha malalamiko ya kisheria kuhusu busu hilo siku ya Jumanne.
Sasa ni juu ya mahakama kuwasilisha mashtaka rasmi dhidi ya mwenye umri wa miaka 46.
Malalamiko ya Hermoso yalikuwa ya unyanyasaji wa kijinsia lakini mwendesha mashtaka Marta Durantez Gil pia ameongeza shtaka la kulazimisha wakati akiwasilisha katika mahakama kuu.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya mwendesha mashtaka ilisema Hermoso alimwambia Gil kwamba jamaa zake walikumbana na shinikizo kutoka kwa Rubiales na “msafara wake wa kitaalamu” kusema kwamba “alihalalisha na kuidhinisha kilichotokea”.
“Waendesha mashtaka wanaomba Luis Rubiales ahojiwe kama mshtakiwa na Jenni Hermoso kama mwathiriwa,” ofisi ya mwendesha mashtaka iliongeza.
Pia inaomba taarifa zikusanywe kutoka kwa mamlaka nchini Australia – ambapo tukio hilo lilifanyika..
Waendesha mashtaka wa Uhispania walifungua uchunguzi wa awali mnamo tarehe 28 Agosti, wakiangalia kama tukio hilo ni sawa na uhalifu wa unyanyasaji wa kijinsia.
Wakati huo, mahakama kuu ya uhalifu ya Uhispania ilisema ilikuwa ikifungua uchunguzi wake kwa kuzingatia “hali isiyo na shaka” ya taarifa za Hermoso mwenye umri wa miaka 33, ikisema ni muhimu “kubainisha umuhimu wao wa kisheria”.
Rubiales amekataa kujiuzulu kama rais wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) tangu tukio hilo, na kuuambia mkutano mkuu usio wa kawaida “Sitajiuzulu, sitajiuzulu,” na kudai “mauaji ya kijamii yanafanyika”.
Shirikisho la soka duniani Fifa lilimsimamisha kwa muda Rubiales na kumfungulia mashtaka ya kinidhamu.