Katika habari kubwa za wiki hii ni pamoja na hii ya hisa za Kampuni ya Apple ya Marekani kushuka kwa asilimia 2.9 kutokana na ripoti za mipango ya China kupiga marufuku matumizi ya simu za Kampuni hiyo (iPhones) kwa Mashirika na Kampuni za kiserikali na kupelekea wasiwasi kwa Wawekezaji juu ya uwezo wa Kampuni hiyo kuendelea kufanya biashara katika uchumi wa pili kwa ukubwa duniani (China).
Apple imepoteza takriban dola Bilioni 200 ndani ya siku mbili baada ya tamko hilo la China, Taifa ambalo ndilo soko kubwa zaidi la nje kwa bidhaa za Kampuni hiyo ambapo mauzo yaliyofanyika Nchini humo yaliwakilisha karibia moja ya tano ya mapato yote ya kampuni hiyo mwaka jana.
CNN wameripoti kuwa japo Apple huwa haisemi ni Nchi gani zimeongoza kwa kununua simu zake, Wachambuzi katika kampuni ya utafiti ya TechInsights wanakadiria kuwa kulikuwa na mauzo makubwa ya iPhone nchini China kuliko hata Marekani kwenyewe mwaka uliopita huku ikikumbukwa kwamba Apple inatengeneza iPhones zake nyingi katika Wiwanda vya China.
Wachambuzi wa Benki ya Amerika Alhamisi wiki hii walisema kuwa uwezekano wa kupiga marufuku iPhone umekuja kutokana na ujio wa simu mpya na ya hali ya juu iliyotengenezwa na Kampuni ya China ya Huawei.