Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya hospitali ya Makuyuni iliyopo katika Wilaya ya Korogwe, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 18 tangu kuanzishwa kwake.
Msaada huo wa Vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 10, umekabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya wa Korogwe Mhe. Jokate Mwegelo na Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Masoud Mrisha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa.
Akiongea katika makabidhiano hayo, Bw. Mrisha amesema TPA imeona itoe msaada wa vifaa tiba hivyo ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora ya matibabu.
Naye Mhe. Jokate Mwegelo ameishukuru TPA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta mbalimbali hususani afya kwa lengo la kusogeza huduma za afya kwa Wananchi.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ametoa rai kwa wadau mbalimbali wajitokeze kuiunga mkono serikali katika kuboresha huduma za kijamii kama ilivyofanywa na TPA.