Luis Rubiales amejihuzulu baada ya kitendo cha kumbusu Jenni Hermoso, wakati timu ya taifa ya Uhispania walipoibuka washindi wa Kombe la Dunia la Wanawake.Kitendo kilichoibua maswali mengi na kukashifiwa vikali.
Jenni Hermoso,kupitia mtandao wake wa Instagram ameonyesha kutoridhishwa na kitendo hicho na kusema kuwa busu hilo halikuwa la maafikiano na hivyo wiki iliyopita siku ya jummane aliwasilisha malalamiko ya kisheria .
Timu hiyo ya wanawake ya Hispania iliibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya England na kufanikiwa kuwa mabingwa wa Kombe la Dunia.
Rubiales katika taarifa yake amesema kuwa hawezi kuendelea na kazi yake na kwamba amewasilisha kujiuzulu kwake kwa kaimu rais wa shirikisho Pedro Rocha.
Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF) limethibitisha taarifa hiyo jana usiku na kubaini kuwa amejiuzulu pia katika wadhifa wake kama makamu wa rais wa shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA).
Awali Rubiales alikataa kujiuzulu na kusema mchezaji huyo wa kike aliridhia kitendo hicho, madai ambayo Hermoso aliyakanusha.
Busu hilo lilizua mzozo kwenye soka la Uhispania katika wiki za hivi karibuni na kufunika ushindi wa Uhispania wa Kombe la Dunia, huku Rubiales akipuuza wito wa mara kwa mara wa kujiuzulu.