Takriban watu 26 wanaripoti kuaga dunia na wengine hawajulikani walipo baada ya kivuko kuzama kaskazini mwa eneo la katikati mwa Nigeria.
Maafisa wa serikali ya Nigeria wameziambia duru za habari kwamba, ajali hiyo ilitokea Jumapili ya jana. Hii ni ajali ya pili kubwa kutokea kwenye eneo hilo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Bogoli Ibrahim, msemaji wa gavana wa jimbo la Niger amesema kwamba ferry hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya watu 100 wakiwemo wanawake na watoto kwenye eneo la Mokwa.
Waliokuwa kwenye ajalii ya ferry hiyo walikuwa wakivuka bwawa kubwa wakielekea kwenye mashamba yao, ameongeza Ibrahim. Watu 26, wengi wao wakiwa watoto na wanawake wamethibitishwa kufa, huku wengine zaidi ya 30 wakiokolewa.
Shughuli za uokozi zinaendelea zikiongozwa na Idara ya dharura ya jimbo la Niger, ikishirikisha polisi wa majini pamoja na wapiga mbizi.
Mwezi Juni mwaka huu, takriban watu 150 walipoteza maisha baada ya mashua waliyokuwa wamepanda kupinduka katika jimbo la Kwara, magharibi mwa Nigeria.
Ajali za mashua na boti za abiria huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria na katika nchi nyingine za Afrika hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mashua hizo kuwa kuukuu na kubeba abiria kupita idadi inayoruhusiwa.
Kwa kuhofia magenge ya wenye kujihami kwa silaha raia wengi wa Nigeria wanatumia usafiri wa boti lakini pamoja na hilo msongamano na matengenezo duni ni chanzo cha vyombo vingi vya majini kusababisha ajali.