Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, zaidi ya watu 300,000 huko Marrakesh na viunga vyake wameathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Morocco.
OCHA imesema: “inafuatilia kwa karibu hali hiyo na iko tayari kuunga mkono juhudi”.
Katika taarifa ya awali, Umoja wa Mataifa ulisema uko tayari “kuisaidia serikali ya Morocco katika juhudi zake za kuwasaidia watu walioathirika”.
Waokoaji wanaendelea kuhangaika kutafuta manusura waliofukiwa na vifusi baada ya tetemeko hilo kubwa la ardhi lililoua zaidi ya watu 2,000.
Wakati huo huo operesheni ya kuwaokoa manusura wa janga hilo la tetemeko la ardhi inaendelea huku ikikabiliwa na changamoto.
Caroline Holt wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu amesema kuwa bado changamoto zinazowakabili waokoaji ni kubwa. Mashine nzito zinahitajika ili kusafisha njia kwa jamii zilizoathirika zaidi katika Milima ya Atlas, aliongeza.
Kuna hofu idadi ya vifo kuongezeka kutoka 2,000 ya sasa hasa katika maeneo ya milimani ambapo kufikika imekuwa changamoto huku wengi huko wakihitaji usaidizi.
Huko Marrakesh, maelfu ya watu wamekuwa wakitumia usiku wa pili kwenye maeneo ya wazi kulala. Maeneo ya mapumziko, maeneo ya kuegesha magari na viwanja vya umma vimejazwa na idadi kubwa ya watu wa kila rika wakijilaza kwenye mablanketi. Wachache wanaonekana kulala, wengi wako macho wakitafakari na kuhuzunika.