Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye alizungumzia “janga ambalo linatuathiri sisi sote”, alionyesha kuwa Paris “imekusanya timu zote za kiufundi na usalama ili kuweza kuingilia kati wakati mamlaka ya Morocco itaona kuwa ni muhimu”.
Timu ya wazima moto wa kujitolea wa Ufaransa kutoka eneo la Lyon (katikati-mashariki) tayari wamewasili Morocco siku ya Jumapili na watashiriki katika shughuli za uokoaji karibu kilomita hamsini kutoka Marrakech, kulingana na mamlaka ya mkoa huo.
Uhispania imetangaza kuwa ilituma timu ya waokoaji 56 nchini Morocco siku ya Jumapili, baada ya kupokea ombi rasmi la usaidizi kutoka Rabat. Ndege ya kijeshi ya A400 iliruka kutoka kambi ya Zaragoza (kaskazini-mashariki) ikiwa na timu ya waokoaji kuelekea Marrakech “kusaidia katika utafutaji na uokoaji wa manusura”, imesema Wizara ya Ulinzi ya Uhispania.
Kitovu cha tetemeko hili la ardhi, la ukubwa wa 6.8 kwenye kipimo cha Richter kulingana na Taasisi ya Marekani ya Jiofizikia (USGS), kinapatikana kusini magharibi mwa Marrakech, kilomita 320 kusini mwa mji mkuu Rabat.
Uswisi ilijitolea kutoa makazi ya muda, vifaa vya kutibu na usambazaji wa maji, vifaa vya usafi wa mazingira na vifaa vya usafi. Uwasilishaji wa vifaa hivi utaambatana na wataalam kutoka Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Uswisi (CSA). Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswizi ilisema Jumamosi jioni kwamba ilikuwa bado haijapata jibu la pendekezo hili.
Ulinzi wa Ubelgiji ulitangaza Jumamosi kuwa huduma ya uratibu wa misaada ya dharura nje ya nchi (B-Fast) ilianzishwa ili kujibu maombi ya usaidizi kutoka kwa mamlaka ya Morocco.
Italia ilitoa msaada kutoka kwa kikosi chake cha ulinzi wa raia na wazima moto, huku Kanisa Katoliki la Italia likituma euro 300,000 kupitia shirika la Caritas Italia.
Rais wa Italia Sergio Mattarella Jumamosi alisisitiza “utayari wa Italia kuchangia kazi ngumu ya uokoaji.”
Uturuki ilipendekeza siku ya Jumamosi kutumwa kwa waokoaji 265 na mahema 1,000, bila majibu kutoka mamlaka ya Morocco.
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki amebaini kuwa nchi yake “iko tayari kutoa usaidizi unaohitajika, ikiwa ni pamoja na timu ya uokoaji”.