Mkurugenzi mkuu, watendaji wote na wafanyakazi wote wa Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni (ICESCO) lenye makao yake makuu mjini Rabat watakuwa wakitoa asilimia 10 ya mishahara yao kuwasaidia wahanga wa tetemeko la ardhi.
Kurugenzi Kuu ilisema katika taarifa yake kwamba fedha hizo zitahamishiwa kwenye akaunti maalum ya Benki ya Al-Maghrib, iliyoombwa na Mfalme Mohammed VI, ili kupokea michango ya mshikamano wa hiari.
“Mnamo Septemba 10, 2023, ICESCO pia ilizindua msafara wa misaada kutoka makao makuu yake huko Rabat kuelekea mikoa iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi. Msafara huu unajumuisha mahema, blanketi na vyakula vya kimsingi … ukisindikizwa na madaktari ambao watasaidia kutoa huduma kwa waliojeruhiwa,” ilisema.
Kwingineko pia Christopher Rassi, mkuu wa wafanyikazi katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, ameiambia Al Jazeera kwamba msaada na uhamishaji wa matibabu unaendelea kwa sasa.
“Tunahitaji kusaidia wale wanaohitaji msaada wa kisaikolojia, makazi ambayo yanaweza kutolewa hivi sasa, chakula, maji safi na msaada mwingine wa afya, pia usafiri wa hospitali – na hiyo inafanywa na mamlaka, wafanyakazi wa kujitolea na wafanyakazi wa Red. Crescent na wengine – uhamishaji, na pia mazishi ya heshima,” Rassi alisema.