TAASISI za serikali zimetakiwa kushirikiana na Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kikosi namba 835 Mgambo Kabuku iliyoko wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, kwenye suala la kilimo cha zao la Mkonge ili iweze kufanikiwa kwa haraka katika harakati za kukuza zao hilo la kimkakati.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi, kambi ya Mgambo, kikosi namba 835, operesheni ya miaka 60 ya JKT, ambapo amewapongeza kwa kujiongezea kipato na uzalishaji wenye tija.
“Na niwaagize wale wote wanaopaswa kushirikiana nanyi, taasisi za serikali waje kwa ukaribu sana ili mipango yenu mliyonayo iweze kufanikiwa kwa haraka, kwahiyo namuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hii na timu yake wafike hapa mkae nao mpange” amesema
“Serikali imeleta vifaa vya kisasa, vikiwemo vya kupimia udongo kwa garama kubwa, hivyo nendeni mkavitumie kuhakikisha kwamba kilimo mnachokifanya kiwe cha kisasa lakini pia kiwe cha mfano, nataka jeshi lenyewe sasa lioneshe kuwa tunaweza kutumia kilimo kwa kuwakwamua wananchi wetu kiuchumi” amesisitiza.
Aidha Wakili Msando amelipongeza jeshi hilo kwa namna lilivyowalea vijana kwani anaamini kwamba wameweza kutambua uzalendo wao kwa nchi yao, lakini pia aliwaasa vijana hao kuwa nidhamu ndiyo kitu pekee muhimu itakayowalea kokote waendako baada ya kupatiwa mafunzo hayo.
Kaimu Mkuu wa kikosi cha 835 KJ Mgambo JKT,Raymond Mwanry alisema mafunzo hayo yana lengo la kuwajenga vijana utayari wa kukitumikia taifa lao na kuwa wazalendo.