Shughuli za wanajeshi 400 wa Ufaransa nchini Gabon, zilizositishwa baada ya mapinduzi ya Agosti 30 huko Libreville, zimeanza hatua kwa hatua nchini humo, Wizara ya Majeshi ya Ufaransa imetangaza siku ya Jumatatu. “Hatua zinaendelea polepole, kwa kesi baada ya kesi,” wizara imesema.
“Kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo, ni wanajeshi wanaofanya mazoezi na ambao wamekuwa pamoja na jeshi la Gabon. Kwa sasa, shughuli zao zimesitishwa wakati wakisubiri hali ya kisiasa ikiwa sawa “, alisema Waziri wa Majeshi wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, katika mahojiano na Gazeti la Le Figaro Septemba 1.
Bw. Lecornu alitaka kutofautisha mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon na yale ya Niger mnamo Julai 26.
“Ufaransa inalaani vitendo vyote vya nguvu (…) Hata hivyo, hatuwezi kufananisha hali ya Niger, ambapo askari walimpindua rais aliyechaguliwa kihalali, na ile ya Gabon, ambapo nia iliyowekwa na jeshi ni kutofuata sheria ya uchaguzi na Katiba.Kwa sababu kwa kweli, kuna mashaka juu ya ukweli wa uchaguzi wa nchi hii”, amebaini.
“Wanajeshi wa Ufaransa nchini Gabon” wanashiriki katika ulinzi wa raia wa Ufaransa, wako tayari kusaidia operesheni na kushirikiana na majeshi ya kitaifa ya Gabon na nchi jirani kama vile Cameroon kwa mazoezi au mafunzo.