Kiungo wa Juventus Paul Pogba amesimamishwa kwa muda kutocheza kwa sababu ya kosa la matumizi ya dawa za kusisimua misuli.
Mahakama ya kitaifa ya kupambana na dawa za kusisimua misuli ya Italia (Nado) ilisema kuwa Pogba alirejesha kipimo cha testosterone baada ya ushindi wa 3-0 wa Juve dhidi ya Udinese mnamo tarehe 20 Agosti.
Mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa Pogba, 30, alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hatumiwi lakini alichaguliwa kwa bahati nasibu kwa ajili ya uchunguzi baada ya mechi.
Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, anaweza kupigwa marufuku kati ya miaka miwili na minne.
Juventus ilisema katika taarifa: “Klabu ya Soka ya Juventus inatangaza kwamba leo, 11 Septemba, 2023, mchezaji wa mpira wa miguu Paul Labile Pogba alipokea agizo la kusimamishwa kwa tahadhari kutoka kwa Mahakama ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa zinazopigwa marufuku michezoni baada ya matokeo ya vipimo vilivyofanywa tarehe 20 Agosti, 2023.
“Klabu inazingatia hatua zinazofuata za kiutaratibu.”
Nado imesema Pogba alikiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli walipopata dutu iliyopigwa marufuku “metaboli za testosterone zisizo asilia”
Testosterone ni homoni ambayo huongeza nguvu kwa wanariadha.
Pogba ana siku tatu kufanya uchambuzi wa kupinga matokeo kwa Nado.
Juventus ilimsajili tena Pogba kwa mkataba wa miaka minne Julai 2022 baada ya mchezaji huyo kumaliza mkataba wake na Manchester United na kuondoka kama mchezaji huru.