Shirika la Mpango wa Chakula Duniani mapema leo limesema kwamba kupungua kwa ufadhili kumelazimisha kupunguza kwa kiasi kikubwa mgao katika mataifa mengi , likionya kwamba watu milioni 24 huenda wakakumbwa na uhaba wa chakula.
Shirika hilo limesema limekuwa likijitahidi kukidhi mahitaji ya kimataifa ya msaada wa chakula huku likikabiliwa na upungufu wa ufadhili wa zaidi ya asilimia 60 mwaka huu na ambao ni wa juu zaidi katika historia yake.
“Kwa mara ya kwanza kabisa, WFP imeona michango ikipungua huku mahitaji yakiongezeka,”ilisema WFP katika taarifa yake.
Hii inaweza kuwa na matokeo mabaya, na wataalam wa WFP wanakadiria kuwa kwa kila asilimia moja ya kupunguzwa kwa msaada wa chakula, zaidi ya watu 400,000 wana hatari ya kuangukia katika viwango vya dharura vya njaa.
Kwa kuzingatia upunguzaji mkubwa unaolazimika kufanya, WFP ilionya katika taarifa kwamba “watu zaidi ya milioni 24 wanaweza kutumbukia kwenye njaa ya dharura katika kipindi cha miezi 12 ijayo, ongezeko la asilimia 50 katika kiwango cha sasa.
Mkuu wa WFP Cindy McCain amesema ufadhili zaidi ni muhimu.
WFP inakadiria kuwa watu milioni 345 duniani kote wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, katika ngazi ya tatu au zaidi katika uainishaji wa Umoja wa Mataifa wa viwango vitano vya uhaba wa chakula, unaojulikana kama IPC.
Milioni 40 kamili kati yao kwa sasa wanachukuliwa kuwa katika viwango vya dharura vya njaa, au IPC level 4, ikimaanisha wanalazimika kuchukua hatua za kukata tamaa ili kuishi na wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo.
“Msaada wa chakula wa shirila la WFP ni njia muhimu ya maisha, mara nyingi ndicho kitu pekee kinachowatenganisha na njaa,” ilisema.