Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ametoa msaada wa kibinadamu kwa Libya baada ya mafuriko makubwa na kusababisha hasara kubwa.
Bw Amir-Abdollahian alisema katika chapisho kwenye X (zamani lilijulikana kama Twitter) siku ya Jumanne kwamba Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran imeeleza kuwa iko tayari kutoa misaada kwa Libya.
Waziri wa Iran pia ameeleza kusikitishwa na maafa hayo na kutuma salamu za rambirambi kwa mamlaka na watu wa Libya pamoja na familia za wahanga.
Iran na Libya hivi karibuni zimepiga hatua kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kikamilifu, huku Tehran na Tripoli zikitangaza mipango ya kufungua tena balozi.
Nchi hizo mbili zina uhusiano wa kidiplomasia, lakini Iran ilifunga ubalozi wake wakati wa uasi dhidi ya kiongozi wa Libya marehemu Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Balozi mpya wa Libya mjini Tehran, Ali Jumaa Hassan Fudail, aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi mjini Tehran mapema Julai.