Zaidi ya nusu ya waathiriwa wa moto wa tarehe 31 Agosti ulioteketeza jengo lililotekwa nyara katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini bado hawajajulikana.
Idara ya Afya ya Gauteng inasema kuwa imewambua waathiriwa 18 zaidi pamoja na wale 12 wa awali, na kufanya jumla ya miili ambayo utambulisho wao umefahamika kufikia 30.
Motalatale Modiba, msemaji wa Idara ya Afya ya Gauteng, alisema kuwa miili ya ziada ilitambuliwa kupitia uchunguzi wa kidijitali wa alama za vidole zilizookolewa za waathiriwa na uchunguzi wa miili na wanafamilia wao.
Hata hivyo, Bw Modiba alifichua kuwa miili 44 kati ya jumla ya 77 iliyopatikana kutokana na moto bado haijatambuliwa.
Aliviambia vyombo vya habari kuwa kwa sasa wanafanya uchanganuzi wa DNA kwenye miili 38 kati ya 44 iliyosalia ili kufichua utambulisho wao. Bw Modiba pia alisema kuwa manusura 27 bado wanatibiwa hospitalini.