Rais wa Urusi Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wamekutana katika ukumbi wa Urusi wa Vostochny mashariki mwa Urusi. Kim Jong-un na Vladimir Putin watafanya mazungumzo kuhusu “mahusiano ya kibiashara” na “mambo ya kimataifa” katika kituo cha kurushia vyombo vya anga, mashirika ya habari ya Urusi yameripoti.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un amewasili katika ukumbi wa Vostochny Cosmodrome mashariki mwa Urusi, ambapo Rais wa Urusi Vladimir Putin yuko. Mkutano wa viongozi hao wawili unaweza kupelekea, kwa mujibu wa Washington, kufikia makubaliano ya uuzaji wa silaha ili kusaidia mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine.
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wamewasili katika ukumbi wa Vostochny Cosmodrome mashariki mwa Urusi, mashirika ya habari ya Urusi yalitangaza Jumatano. Katika mchakato huo, Vladimir Putin alitangaza kuwa Urusi itaisaidia Korea Kaskazini kutengeneza satelaiti, tena kwa mujibu wa mashirika ya Urusi.
Vladimir Putin na Kim Jong-Un watazungumzia kuhusu “masuala nyeti”, kulingana na msemaji wa Kremlin Dmitri Peskov.
Akiwasili nchini Urusi Jumanne jioni, Kim Jong-un anafanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19. Tayari alikuwa amekutana na Vladimir Putin wakati wa safari yake ya awali nje ya nchi, huko Vladivostok mwaka wa 2019. Mahali na tarehe ya mkutano wao, Jumatano hii, vilivuja hivi punde, katika saa za mwisho.