Shirikisho la soka la Morocco limetangaza azma ya kutoa msaada mapato yote yaliyopatikana kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa hapo jana huko Rabat ukiwakutanisha wenyeji Morocco na Burkina Faso msaada utakaowafikia wahanga wa tetemeko la ardhi.
Mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki zaidi ya elfu 40 ulizua hofu ya kuahirishwa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lilitokea huko Morocco mwishoni mwa wiki iliyopita likitajwa kuwa tetemeko kubwa kuliko yote katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
Morocco ikiongozwa na nahodha wake Achraf Hakimi iliwafunga Burkina Faso 1-0 mfungaji wa bao pekee akiwa moja ya nyota waliowika kwenye kombe la dunia mwaka jana Azedine Ounahi.
Rais wa shirikisho la soka la Morocco amethibitisha kuwa fedha zote zilizopatikana kwenye mchezo huo zitaelekezwa kwa wahanga wa tetemeko ikiwa ni mchango wa jamii ya wanasoka kwa juhudi za serikali za kupunguza makali ya janga hili ambalo limesababisha vifo huku mamia ya watu wakiachwa bila makazi.