Nchini Libya, misaada ya kimataifa imefikia maeneo yaliyoharibiwa ili kusaidia timu za uokoaji za ndani. Hii ni baada ya mafuriko makubwa mwishoni mwa juma, ambayo mamlaka inasema, yaliua zaidi ya watu elfu 5200 wakiwemo 3,190 ambao tayari wamezikwa., na elfu 10 bado hawajapatikana na makumi ya maelfu ya wengine kuyahama makazi yao.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Luteni Tarek al-Kharraz siku ya Jumatano aliambia shirika la habari la AFP kwakuwa Miongoni mwao waliofariki walikuwa angalau 400 wageni, wengi wao kutoka Sudan na Misri.
Lakini idadi hiyo iliyokadiriwa ya vifo katika mji wa Derna inasemekana huenda ikaongezeka maradufu na kufikia 18,000 hadi 20,000. Hayo ni kulingana na Meya wa mji wa Derna.
Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) limesema karibu watu 30,000 wameyahama makazi yao huko Derna huku maelfu ya wengine wakipoteza kabisa makazi yao katika miji ya mashariki mwa nchi hiyo. Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 300,000 wameathiriwa na mafuriko hayo.
Mitaa ya miji ilikuwa imefunikwa na matope mazito na kutapakaa miti iliyong’olewa na mamia ya magari yaliyoharibika, mengi yakipinduka ubavu au juu ya paa zao.
Wafanyakazi wa misaada kutoka shirika la usaidizi la matibabu, Médecins Sans Frontières, wanatarajiwa kuwasili jijini leo (Alhamisi), na kujiunga na timu za kukabiliana na dharura.Miili mingi bado haijaopolewa chini ya vifusi au baharini, huku waokoaji wakiomba mifuko zaidi ya mwili.
Chumba cha kuhifadhia maiti na hospitali zimezidiwa na miili.
Daktari wa Libya Najib Tarhoni, ambaye amekuwa akifanya kazi katika hospitali karibu na Derna, alisema msaada zaidi unahitajika.