Serikali nchini Sudan Kusini, imetangaza na kuthibitisha kuwa uchaguzi mkuu wa kwanza ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu tangu nchi hiyo ilipoanza kujitawala mwaka 2011 , sasa utafanyika mwezi Desemba mwaka 2024.
Mwezi wa saba mwaka huu Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir aliahidi kuwa uchaguzi uliocheleweshwa na ambao unatarajiwa kufanywa mwaka ujao utaendelea kama ilivyopangwa na kuwa atagombea kiti cha urais.
Hapo jana Waziri wa Habari Michael Makwei, alisema kuwa uchaguzi huo utafanyika bila ya kuwepo na Katiba mpya.
Aidha, alisema kuwa ni sharti uchaguzi huo ufanyike ili kuwapata wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, wakiwemo wabunge.
Upinzani umekuwa ukimshtumu rais Kiir kwa kutokuwa na utashi wa kisiasa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika, huku Umoja wa Mataifa kupitia mjumbe wake nchini humo Nicholas Haysom akionya kuwa viongozi wa serikali na upinzani wanapaswa kutekeleza mkataba wa amani, na kuandaa uchaguzi huo kama ilivyopangwa.
Ghasia miongoni mwa jamii za Sudan Kusini zinaendelea kuongezeka pamoja na shinikizo la kuongezeka kwa ufinyu wa rasilimali huku maelfu ya watu wakiendelea kuingia nchini humo wakikimbia mapigano katika nchi jirani ya Sudan.