Kim amemwalika Putin kutembelea Pyongyang na Putin amekubali, vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vimeripoti.
Kulingana na shirika la habari la KCNA, Putin alikubali mwaliko huo wakati wa mkutano wao wa Jumatano bila kutaja ni lini ziara inaweza kufanyika.
“Mwishoni mwa mapokezi, Kim Jong Un alimwalika Putin kwa adabu kutembelea DPRK [Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea] kwa wakati unaofaa,” KCNA ilisema.
“Putin alikubali mwaliko huo kwa furaha na alithibitisha nia yake ya kuendeleza historia na utamaduni wa urafiki wa Urusi-DPRK,” iliongeza.
lakini Balozi wa Urusi nchini Marekani Anatoly Antonov alikemea wasiwasi na ukosoaji wa mataifa ya Magharibi juu ya mkutano wa kilele wa Rais Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, akisema Marekani haina haki ya kuingilia kati.
“Marekani haina haki ya kutufundisha jinsi ya kuishi,” Antonov alisema kwenye Facebook akijibu swali la vyombo vya habari kuhusu ziara hiyo iliyofanyika Mashariki ya Mbali ya Urusi siku ya Jumatano.
“Urusi ikiwa nchi yenye nguvu ya nyuklia inayowajibika na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaweza kuamua kwa uhuru ni nani wa kushirikiana naye,” alisema.
Washirika wa nchi za Magharibi wameeleza kusikitishwa na mkutano wa hivi punde kati ya Putin na Kim, huku Ikulu ya Marekani ikieleza wasiwasi wake kwamba mazungumzo hayo ya faragha yatalenga kubadilishana silaha na teknolojia kwa madhumuni ya kijeshi. Urusi na Korea Kaskazini zilikanusha madai hayo.
Jana, Putin alisema mazungumzo yaligusa uwezekano wa “ushirikiano wa kijeshi” kati ya nchi hizo mbili lakini akakubali kuwa kuna mipaka kwa kipengele hicho cha uhusiano.
Urusi ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limepitisha maazimio ya kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini kwa majaribio yake ya makombora na mpango wa nyuklia.
Kim Jong Un wa Korea Kaskazini na Vladimir Putin wamejadili “uwezekano” wa ushirikiano wa kijeshi, katika mkutano uliochunguzwa kwa kina kuhusu makubaliano ya silaha yanayoshukiwa.
Bw Putin pia alisema ataisaidia Pyongyang kutengeneza satelaiti.
Marekani inasema Moscow inanunua silaha kwa ajili ya vita vyake dhidi ya Ukraine, na kuonya msaada wowote utakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Mkutano wa Jumatano kati ya tawala mbili zilizowekewa vikwazo, ambao ulijumuisha maafisa wakuu kutoka pande zote mbili, ulifanyika wakati uhusiano wao na nchi za Magharibi uko duni kabisa.
Akinukuu uhusiano wa kihistoria kati ya Umoja wa Kisovieti na Korea Kaskazini, Bw Putin alimkaribisha mwenzake kwa methali ya Kirusi “rafiki wa zamani ni bora kuliko wawili wapya”.
Bw Putin pia alisema “watajadili mada zote” alipoulizwa ikiwa atazungumza na Bw Kim kuhusu mpango wa silaha.