Meya wa mji wa Derna, mashariki mwa Libya amesema huenda idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na athari za kimbunga kikali kilichoikumba nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikapindukia watu 20,000.
Abdulmenam al-Ghaithi amenukuliwa akisema hayo na kanali ya televisheni ya Al Arabiya na kuongeza kuwa, “Kutokana na ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na mafuriko katika wilaya kadhaa, yumkini watu kati ya 18,000 na 20,000 wamepoteza maisha.”
Al-Ghaithi ameongeza kuwa, mji wa bandari wa Derna wa mashariki mwa Libya ulikuwa na wakazi 125,000 kabla ya kutokea majanga hayo ya kimaumbile, na kwamba huenda umepoteza watu zaidi ya 20,000.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, takriban watu 5,500 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 10,000 hawajulikani walipo hadi hivi sasa baada ya Kimbunga cha Daniel kuyapiga maeneo ya mashariki mwa Libya siku ya Jumapili na kusababisha mafuriko makubwa.
Kimbunga hicho pia kilisababisha kukatika kwa mawasiliano, kuanguka kwa nguzo za umeme na miti na mafuriko kusambaa pia katika miji mingine. Maeneo yote ya mji wa Derna, mashariki mwa nchi hiyo yamemezwa na maji sambamba na wakazi wa maeneo hayo.