Hunter Biden, mtoto wa Joe Biden, amefunguliwa mashtaka ya shirikisho Alhamisi kwa makosa matatu yanayohusiana na kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Mashtaka mawili yanahusishwa na ukweli kwamba alijaza fomu akidai kwamba hakutumia dawa haramu aliponunua bastola ya Colt Cobra mnamo mwezi Oktoba 2018, ambayo ilikuwa ya uwongo, kinaeleza kwa kina kituo cha NBC News cha Marekani. Shtaka la tatu linahusiana na kumiliki silaha huku akitumia dawa za kulevya.
Ulaghai wa kodi…
Mtoto wa rais wa Joe Biden kutoka chama cha Democratic, pia anashukiwa katika kesi ya ulaghai wa kodi. Alifikia makubaliano ya awali ya hatia mnamo mwezi Juni na mwendesha mashtaka David Weiss huko Delaware, jimbo la nyumbani la familia ya Biden, ambayo yalimruhusu kukwepa jela na kesi ngumu. Lakini mwezi Julai, jaji alitilia shaka uhalali wa mpango huo, ambao ulibatilishwa. Baadaye alikana kosa la kukwepa kulipa kodi.
Mwendesha mashtaka maalum alisema mnamo mwezi Agosti kwamba alifunga uchunguzi wa ulaghai wa kodi huko Delaware lakini akasisitiza kwamba utafunguliwa mashitaka tena katika majimbo mengine. Hunter Biden, wakili na mtetezi, anashutumiwa kwa kushindwa kuwasilisha kodi yake mnamo mwaka 2017 na 2018 kwa mapato ya jumla ya dola milioni 1.5.