Utawala wa Kremlin umesema hakuna makubaliano yoyote ambayo yametiwa saini wakati wa ziara ya kiongozi wa Korea Kaskazini nchini Urusi.
“Hakuna makubaliano yametiwa saini na hakuna mpango wa kufanya hivyo” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari.
Matamshi ya Kremlini yanakuja wakati huu Washington ikieleza kuwa huenda nchi hizo mbili zinapanga kuingia katika makubaliano kuhusu silaha.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong aliaanza ziara yake ya kikazi nchini Urusi Jumanne ya wiki hii.
Katika kikao na rais Vladimir Putin siku ya Jumatano, viongozi hao wawili walibadilishana zawadi na silaha, suala ambalo mataifa ya Magharibi yanasema linatuma ishara.
Wakati wa kikao cha viongozi hao wawili, rais Putin alizungumzia umuhimu wa ushirikiano na Korea Kaskazini akieleza uwezekano wa ushirikiano wa kijeshi licha ya Pyongyang kukabiliwa na vikwazo vya kimataifa.
Katika taarifa yake ya Alhamisi ya wiki hii, Utawala wa Kremlin ulitangaza kuwa rais Putin alikuwa amekubali ombi la Kim Jong kuzuru Korea Kaskazini, bila ya kutoa tarehe kamili ya mwaliko huo.