MAHAKAMA ni chombo muhimu katika mchakato wa ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema.
Dkt. Mduma ameyasema hayo jijini Mwanza Septemba 15, 2023, wakati akifungua kikao kazi cha kimkakati baina ya WCF na Watendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Kanda ya Ziwa na Wakurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ili kuwajengea uelewa wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Alisema, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuzitaka taasisi za umma kuongeza ufanisi na ubora wa utoaji huduma kwa wananchi ambapo kikao kama hiki kilifanyika Juni 9, 2023 mjini Bagamoyo na kiliwakutanisha watendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi kanda ya Dar es Salaam na Pwani na wale wa CMA Kanda ya Dar es Salaam.
“Kwa hivyo Mahakama na CMA ni wadau muhimu katika utekelezaji wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi lakini pia tunajenga uelewa wa pamoja, kikao kazi hiki, kitaleta manufaa makubwa ikiwemo kuimarisha mahusiano, kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia kwenye kukuza uchumi wa nchi yetu.” Alifafanua Dkt. Mduma.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina ameipongeza Menejimenti ya WCF kwa kuwa tayari kushirikiana na Mahakama pamoja na taasisi zinazohusu utatuzi wa migogoro ya kazi.
Alisema, mafunzo hayo yatasaidia sana taasisi hizo kubadilishana uzoefu kwenye mambo ya sheria zinazohusu ulipaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kuugua wakiwa kazini au kwa familia za wafanyakazi wanaofariki kutokana na ajali wakiwa kwenye ameneo yao ya kazi.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu alifanya ugatuzi kwa kuelekeza Waheshimiwa Majaji wote wa Mahakama Kuu ya Tanzania Manibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wote sehemu ambazo hazina Masjala ya za Mahakama Kuu kushughulikia mashauri ya Kazi, hivyo niliwaomba WCF watuandalie mafunzo mengine ya kikanda na nashukuru leo tuko hapa Mwazna.”
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi CMA, Bw. Thomas Malekela, alisema tume inashughulikia na haki zilizovunjwa mahali pa kazi.
“Mfanyakazi anaweza akalalamika juu ya mshahara ambao kwaweli si wenyewe, anazungumzia mshahara pamoja na mamslahi, mimi nikatoa uamuzi kuwa mshahara wako halisi ni huu, hivyo WCF itatumia uamuzi huo wa CMA ambayo ndiyo itatumika katika kutekeleza jukumu lake la kulipa fidia.” Alifafanua Bw. Malekela.