Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, mapambano mapya yanayoendelea katika mkoa wa Darfur Kusini nchini Sudan, haswa mjini Nyala, yamesababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.
OCHA imesema watu zaidi ya milioni 5.1 wamekimbia makazi yao tangu katikati ya mwezi Aprili wakati mapambano nchini Sudan yalipotokea, na kati ya watu hao, zaidi ya milioni moja wamelazimika kutafuta hifadhi nje ya nchi.
Pia Ofisi hiyo imesema watoto wasiopungua 435 wameripotiwa kuuawa na wengine 500 wamekufa kutokana na njaa, ingawa idadi halisi ni kubwa zaidi.
Ofisi hiyo imesema kuwa washirika wa kibinadamu wameongeza juhudi na wanaendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji makubwa licha ya uhaba wa fedha, huku watu milioni 3.5 wakipokea msaada tangu mwezi Aprili.