Mwendesha mashtaka wa serikali nchini Gabon amesema mtoto wa kiume mkubwa wa rais aliyeondolewa madarakani, Ali Bongo, na washirika wake kadhaa wa kisiasa wamefunguliwa mashtaka ya uhaini na rushwa.
Mwanawe mkubwa wa Bongo, Noureddin Bongo Valentin na msemaji wa zamani wa rais Jessye Ella Ekogha, pamoja na watu wengine wanne wa karibu wa kiongozi aliyeondolewa madarakani, “wamefunguliwa mashtaka na kuwekwa kizuizini kwa muda,” alisema mwendesha mashtaka wa Libreville Andre-Patrick Roponat.
Bongo, 64, ambaye alitawala nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya katikati mwa Afrika tangu 2009, aliondolewa madarakani na viongozi wa kijeshi mnamo Agosti 30, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais.
Matokeo hayo yalitajwa kuwa ni udanganyifu na upinzani na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi, ambao pia wameutuhumu utawala wake kwa ufisadi ulioenea na utawala mbaya.
Siku hiyo hiyo ya mapinduzi, askari walimkamata mmoja wa wana Bongo, maofisa waandamizi watano na mkewe Sylvia Bongo Valentin.
Televisheni ya Taifa ilionesha picha zake na baadhi ya washirika wa karibu wa baba yake mbele ya masanduku ya pesa ambayo ilisema yalikuwa yamenaswa kutoka kwa nyumba zao.
Wenyewe hawajazungumzia lolote kuhusu tuhuma hizo.
Jeshi lilichukua mamlaka mara baada ya Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Gabon.
Amekuwa ofisini tangu mwaka 2009 alipomrithi baba yake ambaye alitawala nchi hiyo kwa miaka 41.