Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo September 20, 2023 amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na amesema kwamba Serikali imedhamiria kuwa Mzalishaji mkubwa wa nishati na kuwa na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada itauzwa nje ya Nchi.
Akiongea baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika Jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema “Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe Wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya Nchi.
Amesema Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua ambapo amesema katika kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha Viongozi na Wadau kutoka katika Mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo pia kuzisisitiza Nchi zote Wanachama kuhakikisha Taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo katika Sekta za Nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye Sekta hiyo.