Jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Kano, Jumatano lilitangaza marufuku ya kutoka nje ya saa 24, baada ya mahakama kubatilisha uchaguzi wa mgombeaji wa upinzani kama gavana, na kumtangaza mfuasi wa chama cha Rais Bola Tinubu kuwa mshindi halali.
Polisi wa Kano, jimbo ambalo lina idadi kubwa zaidi ya wapiga kura waliojiandikisha, walisema katika taarifa kwamba wanaokiuka amri ya kutotoka nje “watakamatwa na kukabiliwa vikali kisheria.”
Kabla ya uamuzi wa mahakama ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilichukua udhibiti wa barabara kuu, katika mji mkuu wa Kano.
Magavana wana ushawishi mkubwa nchini Nigeria, wakisimamia bajeti kubwa kuliko baadhi ya nchi ndogo za Afrika, na umaarufu wao mara nyingi huchangia pakubwa kuhusiana ni nani atakuwa rais.
Uamuzi wa Jumatano wa jopo la majaji watano ulizusha hofu ya kutokea machafuko katika jimbo hilo lenye Waislamu wengi. Kura ya ugavana mwezi Machi ilishuhudia Abba Yusuf wa New Nigerian Peoples Party, chama cha kikanda, akimshinda mgombea wa chama tawala cha All Progressives Congress, Nasiru Gawuna, ambaye alidai kwamba zoezi hilo liligubikwa na udanganyifu.
“Marufuku ya kutotoka nje ilianza saa kumi na mbili jioni siku ya Jumatano, tarehe 20 Septemba (hadi) saa kumi na mbili jioni siku ya Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2023.
Wakiukaji watakamatwa na kufanywa kukabiliana na ghadhabu kamili ya sheria.
“Mwishowe, napenda kuwashukuru watu wote wapenda amani wa jimbo hili na kuwasihi waendelee kutii sheria kwani ni kwa manufaa ya wote tukutane pamoja ili kudumisha sheria na utulivu nchini,” alisema kamishna huyo wa polisi.