Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC utafanyika kama ilivyopangwa mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 na wakati huo huo tunaomba kutekelezwa kwa ombi letu la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Ni miongoni mwa mambo aliyozungumzia Rais wa DRC Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo wakati akihutubia mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 jijini New York, Marekani jioni ya Jumatano Septemba 20, 2023.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwajulisha kuwa uchaguzi wa Rais hadi madiwani utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na tayari Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC, CENI imeshachapisha orodha ya wagombea wa uchaguzi wa ngazi ya kitaifa, majimbo na manispaa,” amesema Rais Tshisekedi.
Taratibu sasa zinaendelea kuhakikisha kuna uwazi, ujumuishi, fursa sawa na uhalali wa chaguzi hizo zijazo.
Zaidi ya yote, mialiko, amesema imepelekwa kwa mashirika ya kimataifa, ya kiraia na taasisi za kimataifa zinazohusika na masuala ya uangalizi wa uchaguzi halikadhalika kusaidia DRC kufanikisha tukio hilo la kidemokrasia.
Ameshukuru wadau, ukiwemo Umoja wa Mataifa ambao amesema wanasaidia kufanikisha mchakato huo adhimu.
Kuhusu ulinzi wa amani ametaka Umoja wa Mataifa kuzingatia barua ya DRC kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya tarehe Mosi mwezi Septemba mwaka huu inayotoa ombi la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu wa 2023 badala ya Desemba 2024.
“Ombi letu hilo linazingatia kwamba kuondoka kwa MONUSCO kutaondoa mvutano na sintofahamu ya sasa kati yake na wananchi. Lakini tayari nimeagiza maafisa wangu kuwa na mazungumzo na UN ni kwa vipi ushirikiano wetu uendelee.